Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza kumaliza mgogoro wa matumizi ya Pori Tengefu la Loliondo (LGCA) ambao umedumu kwa takriban miaka 26.

Desemba 6, mwaka huu, Waziri Mkuu alitangaza msimamo wa Serikali kuhusu eneo hilo kupitia kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa, Manispaa ya Dodoma ili kutoa mrejesho uliofikiwa na Serikali kuhusu utatuzi wa mgogoro huo baada ya kupokea taarifa ya Kamati ya Uchunguzi.

Hatua hii ya kipekee imekuja baada ya mapendekezo ya tume na kamati zaidi ya saba, ya kutengwa kwa eneo la uhifadhi ili kulinda ikolojia ya Serengeti, kushindikana kutekelezwa.

Hata hivyo, bado kuna shaka kama Loliondo itatulia hasa kutokana na madai kwamba mvutano katika eneo hilo umekuwa ukiyanufaisha mashirika yasiyo ya Serikali (NGOs) zaidi ya 30 yaliyoko katika eneo hilo. Tayari kumeripotiwa kuwapo vikao mjini Arusha vyenye lengo la kupinga mpango huu mpya.

Mmoja wa watu wanotajwa kuwa vinara kwenye mgogoro huo, raia wa Sweden, Susanna Nordlund, ameanza kumshambuliwa Waziri Mkuu Majaliwa kupitia mitandao ya kijamii. Nordlund alishafukuzwa nchini mara mbili kwa kupewa PI.

Waziri Mkuu akatangaza msimamo wa Serikali kwa kuridhia mapendekezo ya kuunda chombo maalum kitakachosimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti na kulinda mazingira na eneo mahsusi la mazalia, mapito ya wanyamapori (ushoroba) na vyanzo vya maji.

Akasema: “Baada ya kupitia mifumo mbalimbali, timu ya wataalam ilipendekeza kuwa utumike mfumo maalum utakaounda chombo maalum, kwa kuwa una maslahi mapana kwa pande zote husika na unalenga kuleta amani na kufikia lengo la kuwa na uhifadhi endelevu katika eneo la Loliondo.”

Waziri Mkuu akaiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae muswada ili itungwe sheria mahsusi ya kuwa na chombo maalum au mamlaka ya kusimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia hiyo na kulinda mazingira na eneo hilo.

Ukiacha ushoroba na mazalia ya wanyamapori, eneo linalokusudiwa kutengwa ndilo chanzo cha asilimia 50 ya maji yote yanayoingia katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Waziri Mkuu ameagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae waraka maalum utakaowasilishwa serikalini kupitia Baraza la Mawaziri kuhusu umuhimu wa kutunga sheria mahsusi ya eneo la Loliondo.

Chombo hicho bado hakijapewa jina, lakini chanzo cha habari kilicho serikalini kimesema huenda kikaitwa Loliondo Game Controlled Area Management Authority. Wataalamu wa Serikali wanaendelea na vikao vya kuandaa muswada huo, na miongoni mwa mapendekezo yao yatahusu msimamizi au mamlaka ambayo chombo kinachoundwa kitakuwa chini yake.

“Kinaweza kuwa chini ya Mamlaka ya Ngorongoro, kinaweza kuwa chini ya Tanapa, kinaweza kuwa chini ya TAWA, na pengine kinaweza kujitegemea kwa maana ya kuwa na mamlaka kamili na kuwajibika moja kwa moja kwa Wizara ya Maliasili na Utalii,” kimesema chanzo chetu.

Waziri Mkuu, akasisitiza: “Sheria itakayotungwa ihakikishe inawekewa masharti yanayozingatia maslahi ya jamii iliyopo katika eneo la Loliondo, mila zao na desturi zao pamoja na mahusiano yao na matumizi ya ardhi.”

Alisema kuna ulazima wa kushirikisha wadau wote mara baada ya rasimu ya kwanza kukamilika ili waipitie kwanza. Alisisitiza rasimu ya pili iwe imefanyiwa mapitio na kukamilika ifikapo Februari au Machi, mwakani ili mahitaji ya fedha yaingizwe kwenye Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2018/2019.

Aliwataka Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta zinazohusika na mgogoro wa matumizi ya ardhi ya Pori Tengefu la Loliondo watembelee eneo hilo ili wawe na uelewa mpana kuhusu changamoto za kisekta zilizopo katika eneo husika.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Mawaziri wa Maliasili na Utalii; TAMISEMI; Ardhi na Maendeleo na Makazi; Naibu Mawaziri wa Kilimo; Maji; Mifugo na Uvuvi na Elimu na Mafuzo.

Pia kilihudhuriwa na wakuu wa taasisi za Serikali, wawekezaji walioko Loliondo, uongozi wa Mkoa wa Arusha, madiwani na wananchi kutoka Loliondo.

Desemba, mwaka jana, Waziri Mkuu alifanya ziara ya kikazi wilayani Ngorongoro ambako alipokea taarifa ya kuwapo kwa mgogoro wa matumizi ya ardhi katika Pori Tengefu la Loliondo.

Januari, mwaka huu aliunda Kamati ya Uchunguzi iliyokuwa na wajumbe 27 iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Taarifa kutoka kwenye kikao cha Dodoma zinasema Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya serikali ya Pastoralist Women Council (PWC), Manda Neritiko, aliishukuru Serikali kwa kuwashirikisha wananchi kutafuta suluhu ya mgogoro huo, hatua ambayo alisema haijawahi kufanyika miaka yote ya nyuma.

“Huko nyuma tulikuwa tukipewa maagizo tu, Serikali imeamua hivi, Serikai imesema vile, lakini kwa awamu hii, tumeweza kuitwa kwenye vikao mbalimbali na kutoa maoni yetu na hata kupewa mrejesho,” alisema.

Maanda ambaye hati yake ya kusafiria umezuiwa kutokana na utata wa uraia wake, alimwagiwa sifa na Waziri Mkuu, akimtaja kama mmoja wa watu muhimu katika ustawi wa Loliondo.

Maanda alikuwa mwanachama na diwani wa viti maalumu kupitia CHADEMA kabla ya kurejea CCM.

Je, mgogoro wa Loliondo umefikia tamati?

JAMHURI limedokezwa kuwa hadi wajumbe wanaondoka katika kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu, baadhi yao hawakuelewa hasa chombo kinachoundwa kama ilivyoagiza serikali ni cha aina gani.

Ingawa Waziri Mkuu hakutamka bayana, msimamo huu wa Serikali unarejea kwenye mapendekezo ya wataalamu ya kutengwa kwa eneo maalumu kisheria ili kulinda ikolojia ya Serengeti. Kwa msingi huo, Serikali inatekeleza msimamo wa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, wa kutenga eneo la kilometa za mraba 1,500 kwa ajili ya hifadhi ya vyanzo vya maji, ushoroba na mazalia ya wanyamapori.

Msimamo huo wa Kagasheki ulitenguliwa na Waziri Mkuu wa wakati huo, Mizengo Pinda, na hivyo kuzidi kuukoleza mgogoro huo.

Baada ya mkutano wa Dodoma, baadhi ya viongozi wa NGOs na wenzao wanaopinga mpangi huo, wameonekana kutopea kwenye wingu la sintohafamu; na tayari wameshaanza kufanya vikao kadhaa mjini Arusha na Loliondo.

Kabla ya hapo, Gambo alikuwa akitetea uanzishwaji Eneo la Jumuiya ya Hifadhi (WMA), lakini mapendekezo hayo yakapingwa na wahifadhi. Hata walipokwenda kukabidhi ripoti Dodoma, wahifadhi waliikana na kumweleza Waziri Mkuu kuwa yaliyomo hawayaafiki kwa kuwa si ya kiuhifadhi. Wanaopinga uanzishwaji wa WMA wanatoa sababu zifuatazo:

Mosi, kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji wa WMA, ni lazima kwanza ardhi iwe ya vijiji. Baada ya kuanzishwa kwa WMA, kwa mujibu wa sheria kijiji kinaruhusiwa kujiondoa katika WMA, jambo ambalo kwa Loliondo walisema ni rahisi na ni hatari kwa uwepo wa Hifadhi ya Taifa Serengeti na Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro.

Kumekuwepo na mgongano wa koo za Wamaasai katika eneo la Loliondo kwa muda mrefu. Eneo hilo lina koo kubwa tatu za Puruko, Loitha na Laitayoki. Koo hizi zipo pande zote za mpaka – Tanzania na Kenya. Zimekuwa zikikinzana hata katika kutekeleza shughuli za kimaendeleo. Katika mazingira hayo ni vigumu kwa koo hizi kuwa pamoja na kusimamia eneo moja kwa masilahi mapana ya jamii, taifa na uhifadhi wa maliasili.

Tatu, uwekezaji na rasilimali zilizopo katika vijiji unatofatiana. Baadhi ya vijiji vina wawekezaji wanaofanya shughuli za utalii na kuchangia fedha nyingi katika vijiji. Hivyo, uwepo wa WMA katika eneo la Loliondo utalazimisha mgawanyo sawa wa mapato kwa vijiji vyote, jambo ambalo litasababisha vijiji vyenye mapato makubwa kwa sasa kukataa kuingia katika umoja wa kuanzisha WMA. Mfano ni Kijiji cha Ololosokwan.

Nne, kwa mujibu wa taarifa za tathmini ya WMAs zilizofanywa mwaka 2007 na mwaka 2012, kumekuwapo upungufu mkubwa katika kusimamia na kuendesha hifadhi hizo za jamii. Kati ya hifadhi 22 za jamii zenye hadhi ya Authorized Association (AA) ni WMA moja tu ya Ikona wilayani Serengeti ambayo imeonesha mtazamo chanya katika usimamizi na uendeshaji wake.

Tano, kifungu cha 6(1)(a) cha Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 kinatambua maeneo yaliyohifadhiwa kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha maeneo hayo ikiwemo Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 ambamo mapori tengefu yanatambulika kama hifadhi. Kwa hiyo, eneo la Loliondo ni Pori Tengefu (Loliondo Game Controlled Area (LGCA). Ili WMA eneo hilo lazima lihaulishwe na kuwa ardhi ya vijiji. Mfumo wa WMA ulijadiliwa na kukubaliwa na wawakilishi wa jamii, kama ulivyopendekezwa na Gambo kuwa utakuwa “mfumo maalum”. Umiliki wa ardhi utakuwa wa pamoja, yaani chini ya vijiji na Wizara ya Maliasili na Utalii. Mfumo huu una changamoto kubwa katika mtazamo wa kisheria. Kwa mujibu wa sheria hakuna ardhi inaweza kumilikiwa kwa mfumo huo. Ardhi lazima ihaulishwe kwanza kabla ya kuanzishwa WMA. Ardhi ikishakuwa ya vijiji ni vigumu kuirudisha tena kuwa hifadhi.

Sita, Wilaya ya Ngorongoro ina jumla ya vijiji 72 lakini, kimsingi, hakuna hata kimoja chenye hati ya ardhi. Huko nyuma kulikuwa na vijiji viwili vya Ololosokwan na Ngaresero lakini, mwaka 2014, kupitia Gazeti la serikali Na. 301 la tarehe 22/08/2014, vijiji hivyo viligawanywa, kila kimoja kikatoa vingine. Kijiji cha Ololosokwan kiligawanywa na kutoa vijiji vitatu vya Ololosokwan, Mairowa na Njoroi. Kijiji cha Ngaresero kilitoa vijiji vya Monik na Ngaresero. Hivyo, kimsingi, ukishagawa kijiji na kutoa vijiji viwili au zaidi, hati ya ardhi ya kijiji mama inakuwa haina uhalali tena. Kwa sasa hakuna vijiji vilivyopimwa katika Wilaya nzima ya Ngorongoro.

Please follow and like us:
Pin Share