Nyerere2

 

Katika toleo lililopita niliishia kuchambua maneno ya mwanzo yaliyokuwamo kwenye Katiba Tanganyika ya 1961 mara baada ya Uhuru.
  Maneno ya utangulizi kutoka kwa Mwalimu Nyerere yaliyosomeka hivi: namnukuu, “In particular I trust that the young will take particular note of the preamble, where they will find those high ideals by which one country should always seek to direct itself. The concepts of LIBERTY, OF EQUAL RIGHTS FOR ALL, of an INDEPENDENT JUDICIARY, should inculcate into the youth of Tanganyika from the earliest possible stage. It is the duty of all of us to see that these IDEALS become truly a part of our national life, and not mere catchwords and slogans of no significance” (JK Nyerere Prime Minister – 1961).


  Imenilazimu kunukuu utangulizi huo karibu wote kwa vile nimeshindwa kuutafsiri kisheria maana sahihi ya maneno haya. Lakini la msingi hapa ni kwamba katika Katiba iliyotupatia Uhuru Mwalimu alihimiza vijana kuitafakari kwa kina maudhui yake.
 Mle kuna malengo, kuna mahimizo na kuna miito (slogan) na vidahizo (catchwords) vya kuwasisimua vijana kutafakari hali ya baadaye ya Watanganyika.
  Katiba imesema juu ya haki sawa, imetoa mawazo au dhana (ideals) za Uhuru wa watu, haki na wajibu za watu na Uhuru wa Mahakama.


  La msingi vijana watafsiri hayo kwa manufaa ya wote na ndipo akamalizia kuhimiza wajibu wa kila mmoja wetu kuandaa mazingira ya maisha bora ya kitaifa kwa wananchi wote. Vijana wale wa miaka ile ya 1961 ndiyo wazee wa leo hii.  
  Kwa utangulizi ule, Mwalimu alijionesha moja kwa moja kuwa alikuwa mzalendo. Aidha, aliandaa fikra sahihi kwa vijana kujengwa mawazo yake ya uzalendo, ya kukua pamoja na kujenga Taifa hili katika misingi ya uzalendo. Utaifa ulikuwa umeshakuja wenyewe, uraia ulikuwa ni ‘automatic’ wala haukuhitaji kujengwa lakini UZALENDO ulihitaji ujengeke miongoni mwa raia wa nchi hii. Mahali sahihi pa kuwajenga vijana wote kuwa wazalendo palikuwa katika jando la kitaifa “Jeshi la kujenga Taifa”.


  Sasa kama vijana wote wangepita katika tanuri hili (moulding pot) na wakageuka kuwa kweli wazalendo – UFISADI katika nchi hii ungepitia wapi? Maana ubinafsi ungekomeshwa huko huko jandoni. Lakini wapi! Wapo waliopita jandoni na wapo waliokwepa jando lile na wala hawakupikika na hawakujengeka ndiyo vijana namna hiyo wakawa sugu kwa UZALENDO wakageuka kuelekea kwenye ubepari.
  Mwalimu, kwa kile kipawa chake cha kuona mbali katika maisha ya Watanzania, alikuwa na utamaduni wa kutoa matamshi kuwahimiza vijana wajenge moyo wa kulijenga Taifa hili.
  Oktoba 1966 pale Makao Makuu ya Chama, Lumumba, Mwalimu aliwakemea vijana wa vyuo vikuu wakati huo na  aliwahimiza wananchi kwa maneno haya.
“Enyi wananchi nchi hii tutaijenga kwa moyo, kwa kila mmoja wetu aseme jamani nina kapato fulani sasa nijifunge moja kwa moja pamoja na wenzangu tuijenge nchi yetu”.


Hotuba ile ya Mwalimu ilipewa kichwa “TANZANIA ITAJENGWA NA WENYE MOYO” (maelezo ya Rais Mwl. J. K. Nyerere, Lumumba, DSM Jumapili, uk. 23, 1966). Hapo tujiulize hao wenye moyoni akina nani?
  Haiwezekani kabisa watu namna hiyo wakawa miongoni mwa wale wenye unafsi, wanaojitafutia utajiri kwa njia zozote zile. Lazima watu hao wawe kwanza wazalendo na wenye uchungu na nchi yao, wapenda kujitolea kwa maendeleo ya wananchi wote.


  Mmoja wa watu namna hiyo ni Baba wa Taifa. Hakuwa mbinafsi, hakuwa mpenda kujilimbikizia utajiri, hakuwa na makuu na daima alikuwa mnyenyekevu mbele ya watu. Huko ndiko kuonesha njia wenzako wakufuate, lakini ni wangapi miongoni mwa raia wa nchi hii wamemfuata Mwalimu kimatendo?
  Je, ukipata viongozi, raia wa nchi hii wanaoweza kutamka hadharani eti sh. 10,000,000/- ni fedha za mboga tu, si unajiuliza huyu ni mzalendo? Kama sh. 10,000,000/- ni za kitoweo, je, matumizi mengine yanakuwaje? Uzalendo kamwe haujifikirii nafsi bali unatazama hali ya jamii inayokuzunguka ikoje? Kama raia wengi nchini wangekuwa na uzalendo, kwanza wasingalikwepa ulipaji wa kodi, pili wasingekomba fedha za EPA, wasingeleta akina Richmond kubabaisha umeme wa nchi hii wala wasingethubutu kugawana fedha za escrow kama njugu. Tangu lini mzalendo akasema nilipokea vijisenti kidogo tu! Wala havinibabaishi?


  Mwanzoni mwa makala hii nilisema maneno haya mawili URAIA na UZALENDO hayatumiki kwa usahihi hapa nchini. Mara kwa mara yanabadilishwa (swopped). Uraia ni hali ya kuzaliwa katika nchi na hivyo kila mmoja ana haki ya kuitwa raia wa nchi husika. Uzalendo ni moyo wa uchungu wa nchi, mwananchi anaokuwa nao na ndiyo moyo unaomsukuma kuitetea nchi yake hata ikibidi kufia nchi yake. Huyu asilani hawezi kuihujumu nchi yake, hawezi kuiuza na hawezi kuiibia kwa namna yoyote ile. Je, tunao wazalendo kweli wa namna hiyo? Yale maneno ya kwenye michezo mathalani mpira wa miguu, eti tuwe wazalendo tusiwe na msimamo wa kivilabu vyetu siyo alama ya uzalendo. Uzalendo mtu haibi fedha za milangoni (gate collection) kwa kujifunaisha.


  Kilio changu ni kuwa ndoto za Baba wa Taifa kuwa na Taifa la wajamaa safi hazikufanikiwa. Wameibuka wanyonyaji na kuimba wimbo wa Baba wa Taifa – “Chama chetu cha Mapinduzi chajenga nchi”. Ni kweli chama kina sera ya kujenga nchi lakini je, wanachama wake wote wana moyo huo wa kujenga nchi? Kwa nini wamemgeuka Baba wa Taifa hata kabla hajafa? Wakavuruga miiko ya uongozi na kushabikia ubepari?


Mayahudi enzi za Bwana wetu Yesu Kristo walimshangilia sana siku ile ya Matawi. Walimtandikia nguo barabarani pale Yerusalemu akapita amepanda punda na wakimshangilia kwa matawi ya mitende. (Mat. 21:9 – 11). Baada ya shangwe zile, Mayahudi wale wale waliamua kumsulubu kwa kipigo, dharau na hatimaye walimtundika msalabani. Tunasoma katika maandiko, “Askari mmoja alimchoma kwa mkuki” ndipo tunahitimisha kwa kusoma maandiko yasemayo “wakamtazama yeye waliyemchoma” (Yoh. 19:34 na 37).


 Mimi kwa nukuu hizi napenda kumalizia kwa kusema, uzalendo tulioletewa na Mwalimu hapa Tanzania sote tulifurahia na kushangilia. Lakini tulipoletewa miiko ya uongozi katika Azimio la Arusha, ndipo tulipomgeuka Baba wa Taifa kwa Azimio letu la Zanzibar. Kisha tukamtazama kwa kejeli pale tuliponogewa na ubepari mpaka tukafika hatua ya kufuta miiko yote ya uongozi. Hakuna cha maadili mema hata tukiitwa kwenye Tume yetu ya Maadili ndiyo kwanza tunakejeli uhalali wake na kudai mpaka Mahakama Kuu iamue! Tumefika hapo pa viongozi wakuu wa chama tawala na wajumbe wa NEC kukejeli sera ya chama chao. Huko mimi naita kumtazama yule aliyewaleta hapo walipo. Kwa vile ameshafariki basi tuamini usemi katika ile methali isemayo, “ASIYEKUWAPO NA LAKE HALIPO” (out of sight, out of mind).


 Tungekuwa na chembe za UZALENDO kamwe hali namna hii isingalitokea! Bado natamani kuona Watanzania wa leo tunatambua tofauti kati ya URAIA na UZALENDO. Uraia ni wa kuzaliwa lakini UZALENDO unajengwa na wenye moyo tu.
  Tunasikia viongozi kadhaa wa siasa wakimnukuu Baba wa Taifa na kutamka neno uzalendo, je, miongoni mwa viongozi hao kweli hakuna walioshiriki kuliua lile Azimio la Arusha kwenye kile kikao cha Zanzibar? Watu  namna hiyo ni wazalendo au wasaliti wa Azimio? Mimi mpaka hapo naweza kusema sijui ukweli wa hayo. Ninajua kwa hakika sote tu RAIA wa Jamhuri ya Muungano. Lakini wangapi WAZALENDO ndani ya Jamhuri yetu sijui kabisa. Wewe na mimi tulijiulize, licha ya uraia wetu, je, tu WAZALENDO?

By Jamhuri