Na Edward Kondela, JamhuriMedia, Karagwe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka historia ya kutafsiri ndoto halisi ya wingi wa mifugo nchini katika kubadilisha mfumo wa maisha kwa watanzania kupitia sekta hiyo.

Akizungumza (21.05.2024) wakati wa hafla fupi ya kuwaonesha vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji mifugo kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), inayosimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, vitalu watakavyopatiwa kwa ajili ya ufugaji katika Ranchi za Kagoma na Kitengule zinazosimamaiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe. Julius Laizer amesema Mhe. Rais ameweza kuirasimisha rasmi biashara ya mazao ya mifugo kwa kuwa Sekta ya Mifugo ni muhimu katika maisha ya binadamu.

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika Ranchi ya Kagoma iliyopo Wilaya ya Karagwe mkoani humo ya kuwaonesha vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji mifugo kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), baadhi ya maeneo watakayopatiwa kwa ajili ya vitalu vya kufugia mifugo, Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Mhe. Julius Laizer amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka historia ya kutafsiri ndoto halisi ya wingi wa mifugo nchini katika kubadilisha mfumo wa maisha kwa watanzania kupitia sekta hiyo. (21.05.2024)

Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Laizer amesema ni vigumu kutenganisha biashara yoyote inayohusu chakula cha binadamu isifanikiwe, hivyo kuwataka vijana wa BBT – LIFE kusimamia vyema ndoto na maono ya Mhe. Rais kwa kuwa wapo sehemu sahihi katika kujifunza na kufuga mifugo kibiashara.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi amesema wizara inawaangalia vijana hao kama waleta mapinduzi kwenye Sekta ya Mifugo hivyo imeamua kuwaunganisha na baadhi ya benki zilizopo nchini kupata fursa za mikopo.

Ameongeza kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alianzisha programu hiyo kwa kwa kuitambua Sekta ya Mifugo kama sekta rasmi na kuwaingiza vijana kwenye ufugaji na uvuvi wa kibiashara na kwamba kila mwaka takriban vijana 1,600 wanahitimu kwenye vyuo mbalimbali vya mifugo hivyo serikali imeona haiwezi kuwaacha bila ajira bali wajifunze ufugaji kibiashara.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi akizungumza na kuwaonesha baadhi ya vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji mifugo awamu ya kwanza kupitia Programu ya Jenga kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), vitalu watakavyogaiwa kufanya ufugaji katika Ranchi za Kagoma na Kitengule ambazo ziko chini ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) katika Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, ambapo katika kipindi cha miaka mitano hawatatozwa malipo ya upangaji katika ranchi hizo. (21.05.2024)

Aidha, amesema Mhe. Rais katika diplomasia ya kiuchumi amekuwa akizunguka nchi mbalimbali kutafuta masoko ya mazao ya mifugo na uvuvi ambapo kwa sasa nchi inahitaji wawekezaji wakubwa katika sekta hizo ili kuvipatia viwanda vilivyopo nchini mifugo kwa ajili ya kuchakatwa na kuhudumia masoko ya kimataifa, ambapo pia vijana wa BBT – LIFE wanatakiwa kuwa wawekezaji wakubwa katika Sekta ya Mifugo.

Pia, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Bw. Bwire Mujarubi amesema kwa mujibu wa mwongozo kampuni hiyo imepewa majukumu ya kutenga vitalu kwa vijana wa BBT – LIFE, kupanga vijana hao kwenye vitalu, kuwapatia mikataba wafugaji katika ranchi za NARCO na kuwa miongoni mwa wateja wa mifugo kutoka kwa vijana wa BBT – LIFE watakaopatiwa vitalu katika ranchi hizo.

Amesema licha ya awamu ya kwanza ya BBT – LIFE kuelekea mwishoni ifikapo Tarehe 30 Mwezi Juni mwaka huu, NARCO itaendelea kuwalea vijana hao 161 ambapo kila mmoja atapatiwa ekari 10 bila kulipa gharama za upangaji katika kipindi cha miaka mitano kwenye ranchi za Kagoma hekta 311 na Kitengule hekta 2,000 zilizopo Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Daniel Mushi (mwenye kofia nyeusi) akizungumza na baadhi ya wadau na vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji mifugo awamu ya kwanza kupitia Programu ya Jenga kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), wakati vijana hao wakioneshwa vitalu watakavyogaiwa kufanya ufugaji katika Ranchi za Kagoma na Kitengule ambazo ziko chini ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) katika Wilaya ya Karagwe Mkoani Kagera, ambapo jumla ya vijana 161 watapatiwa vitalu ambapo kila mmoja atapatiwa ekari 10. (21.05.2024)

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Dkt. Pius Mwambene amesema kwa kipindi cha miaka miwili ambacho vijana wa BBT – LIFE wamekuwa wakipata mafunzo katika wakala hiyo wamepata uzoefu mkubwa wa kuandaa miundombinu ya mifugo pamoja na biashara ya mifugo.

Ameongeza kuwa vijana hao wakianza rasmi ufugaji hawataangaika na kwamba watakuwa wakishirikiana na wawekezaji wakubwa waliopo kwenye ranchi za NARCO, huku akibainisha kuwa wakati wa mafunzo vijana hao wamekuwa wakiuza mifugo ndani ya nchi pamoja na nchi za jirani.

Pia, amesema amesema lengo la programu hiyo ni kukuza ufugaji wa mifugo wenye tija kwa kuandaa vijana kuwa wawekezaji wakubwa kwenye sekta hiyo na kwamba programu hiyo kwa sasa itapelekwa kwenye ngazi za serikali za mikoa ili kuwanufaisha vijana wengi zaidi.

Mmoja wa vijana wanaonufaika na programu ya BBT – LIFE Bw. Posper Mugalula amesema wanashukuru kwa kupata fursa ya kushiriki mafunzo ya unenepeshaji mifugo hususan ng’ombe baada ya kumaliza elimu ya vyuo na wapo tayari kuingia rasmi katika ufugaji wa kisasa baada ya kupatiwa vitalu kwenye ranchi za NARCO.

Amewaomba vijana wenzake kushirikiana ili kufikia malengo ambayo serikali imekusudia na kuwa chachu ya vijana wengine kujiunga na mafunzo kwa awamu ya pili na kufuga kibiashara kwa kuwa Sekta ya Mifugo ina soko kubwa ndani na nje ya nchi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) Bw. Bwire Mujarubi akifafanua majukumu iliyopatiwa kampuni hiyo ya kutenga vitalu kwa vijana wa BBT – LIFE, kupanga vijana hao kwenye vitalu, kuwapatia mikataba wafugaji katika ranchi za NARCO na kuwa miongoni mwa wateja wa mifugo kutoka kwa vijana wa BBT – LIFE watakaopatiwa vitalu katika ranchi hizo. Bw. Mujaribu amebainisha hayo wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika Ranchi ya Kagoma iliyopo Wilaya ya Karagwe mkoani humo ya kuwaonesha vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji mifugo kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), baadhi ya maeneo watakayopatiwa kwa ajili ya vitalu vya kufugia mifugo. (21.05.2024)

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikiendesha mafunzo ya unenepeshaji mifugo katika vituo vya Wakala ya Mifugo nchini (LITA) na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE) ili kufikia maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha vijana kufanya ufugaji wenye tija katika sekta za mifugo na uvuvi.

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) Dkt. Pius Mwambene amesema kwa kipindi cha miaka miwili ambacho vijana wa BBT – LIFE wamekuwa wakipata mafunzo katika wakala hiyo wamepata uzoefu mkubwa wa kuandaa miundombinu ya mifugo pamoja na biashara ya mifugo. Dkt. Mwambene amebainisha hayo wakati wa hafla fupi iliyofanyika katika Ranchi ya Kagoma iliyopo Wilaya ya Karagwe mkoani humo ya kuwaonesha vijana wanaohitimu mafunzo ya unenepeshaji mifugo kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT – LIFE), baadhi ya maeneo watakayopatiwa kwa ajili ya vitalu vya kufugia mifugo. (21.05.2024)

By Jamhuri