Na Mwandishi Wetu, Jamhurimedia, Arusha

Tuhuma za kughushi nyaraka, uchepushaji wa makusanyo ya Serikali na ubadhirifu wa fedha za umma zimechukua sura mpya baada ya watumishi wawili kudaiwa kuhusika kutengeneza namba bandia ya mlipakodi na kampuni hewa ya kulipia makusanyo hayo.

Kutokana na uchunguzi huo wa awali kubainisha hilo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TaAKUKURU) Mkoa wa Arusha, imefanya uchunguzi wa mfumo mzima wa malipo ili kubaini makampuni mengine hewa na namba bandia za mlipakodi zilizotumika kuchepusha kodi au mapato yoyote katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Akizungumzia suala hilo leo Mei 27, 2024, Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha Zawadi Ngailo, amesema uchunguzi wa awali umebaini watumishi wawili wa halmashauri hiyo wamehusika kughushi nyaraka ikiwamo kutengeneza namba bandia ya mlipakodi na kutumia kampuni hewa kulipia mapato.

Ngailo ameeleza kuwa kutokana na maelekezo yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda, tayari taasisi hiyo ilikuwa imeshaanza uchunguzi wa awali toka siku ya kwanza walipopata malalamiko hayo.

“Maelekezo yalitolewa kwenye kikao kati ya Mkuu wa mkoa na wafanyabiashara wa utalii Mkoani Arusha na ofisi ilikuwa imeshaanza uchunguzi na uchunguzi huo ulikuwa unahusisha idara ya mapato ( Ushuru wa Huduma ) katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.

” Kwa hiyo hadi sasa uchunguzi umefikia hapo ambapo tumebaini watu wawili kutokana na uchunguzi tuliyoufanya na kuwabaini hao watuhumiwa, inamaanisha tulihoji watu ambao ni mashahidi na pia tuliwahoji na watuhumiwa wenyenye na kuwabaini wawili lakini bado uchunguzi unaendelea”. ameongeza Ngailo.

Aidha kamanda huyo wa TAKUKURI ameeleza kuwa katika uchunguzi huo waliyo ufanya na wanaoendelea kuufanya utakapokamilika hatua itakayo fuata ni kuwafikisha mahakani watuhumiwa wote waliyo husika na ubadhilifu huo wa mamilioni ya fedha.

“Hatua inayofuata tutakapo kamilisha tutawafikisha mahakamani kwa mujibu wa utaratibu na uchunguzi huu unahusisha wale wote waliyokuwa wanahusika na ukusanyaji wa mapato (Ushuu wa Huduma) na lengo la kuchungua ni kuhakikisha wote tulio wabaini wanafikishwa mahakamani” amesema Ngailo.

Ikumbukwe TAKUKURU inafanya uchunguzi huo ikiwa ni agizo la Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kufuatia tuhuma zilizowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Wilbard Chambulo kudai kulipa kodi ya huduma Shilingi milioni 24, lakinii akapewa risiti ya Shilingi milioni 3.6.

Hata hivyo taarifa zimebaini kuwa makampuni hayo bandia yalitengenezwa miezi ya mwishoni mwaka 2022 kitu ambacho Mkurugenzi hivi sasa Juma Hamsini hakuwepo na hakuwa Mkurgenzi wa Jiji la Arusha ijapokuwa watumishi hao walikuwepo katika kitengo hicho.

Pia kufuatia malalamiko ya mfanyabiashara huyo Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Juma Hamsini alitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari juu ya jambo ambalo limeibua mambo mapya hadi kupelekea RC Makonda kutoa tamko la kufanyika uchunguzi huo kwa kupitia TAKUKURU.

Aidha ikumbukwe Juni 13, 2023 Juma Hamsini alikabidhi rasmi Ofisi na kuwa Mkurugenzi mpya wa Halmashauri hiyo ya Jiji la Arusha baada ya kuteuliwa mnamo Juni 7, 2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.