Na Mwandishi Wetu, JamhuriMwdia, Morogoro

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu ameilekeza Bohari ya Dawa (MSD) kuwajali wateja na kuwashirikisha katika suala zima la kuwapa huduma za mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini.

Dkt. Jingu ambaye alifungua rasmi kikao cha ishirini na mbili (22) cha Baraza la Wafanyakazi la MSD mjini Morogoro amesisitiza kuwa, kujali wateja ni msingi wa kuwahudumia wateja kulingana na mahitaji yao.

Aidha, Katibu Mkuu huyo amesisitiza MSD kujiendesha kibiashara na kuwa wabunifu ili kuweza kuleta ufanisi na tija.

Wakati huo huo Mkurugenzi Mkuu wa MSD Ndugu Mavere Tukai ameeleza kuwa MSD ni miongoni mwa taasisi za kimkakati na imeanza kujiendesha kibiashara.

Tukai ameongeza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja, MSD imeweza kuongeza hali ya upatikanaji wa bidhaa za afya kwa kuingia mikataba ya muda mrefu na wazalishaji ambapo upatikanaji wa dawa umeongezeka kutoka asilimia 51 mwaka jana wa fedha, hadi kufikia zaidi ya asilimia 80 mwaka huu. Eneo hili pia linaonekana kwenye kutimiza mahitaji ya wateja ambapo mwaka jana ilikuwa asilimia 44, na hii imeongezeka na kufikia asilimia 78.

Kwa upande wa mauzo, Tukai ameeleza kuwa kuna ongezeko la mauzo ya bidhaa za afya kutoka shilingi 77 bilioni mwaka jana wa fedha, na kufikia shilingi 123 bilioni mwaka huu wa fedha.

Mkurugenzi huyo ameahidi kwamba MSD itaendelea kuboresha kazi zake ili kuimarisha utendaji wa kazi zake

By Jamhuri