Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kibaha
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Pwani kimezitaka halmashauri kuhakikisha maeneo yenye taasisi za umma yanapimwa na kumilikishwa hati ili kuzuia migogoro ya ardhi inayoweza kusababisha upotevu wa mali za serikali.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Pwani, Bumija Senkondo, wakati akichambua ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa baadhi ya halmashauri za mkoa huo katika mkutano wa chama hicho uliofanyika Kibaha.
Senkondo alisema ripoti ya CAG imebaini uwepo wa majengo tisa ya umma yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili katika halmashauri za Kibiti, Mafia na Chalinze ambayo ardhi yake haina hati miliki, hali inayoweza kuyafanya kuingia kwenye migogoro ya ardhi.
Alisema baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wanaweza kujitokeza na kudai umiliki wa maeneo hayo kutokana na kutokuwepo kwa nyaraka rasmi za umiliki, jambo litakalosababisha migogoro isiyo ya lazima kwa taasisi za umma.
Katika hatua nyingine, Senkondo alihoji uuzaji wa viwanja 168 vyenye thamani ya shilingi bilioni 4.09 katika Manispaa ya Kibaha nje ya mfumo rasmi wa TAUSI, akisema hatua hiyo imechochea upotevu mkubwa wa mapato ya serikali.
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, sehemu ya fedha zilizotokana na mauzo hayo, kiasi cha shilingi milioni 481.77, ziliingizwa kwenye akaunti binafsi za watu ambao si watumishi wa halmashauri huku zaidi ya shilingi bilioni 3.61 zikishindikana kuthibitishwa kutokana na kukosekana kwa nyaraka rasmi za malipo na kumbukumbu za benki.
Kutokana na hali hiyo, CHADEMA imetaka mamlaka husika, ikiwemo TAKUKURU, Wizara ya Ardhi na TAMISEMI, kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya watumishi waliohusika, kurejesha maeneo ya umma yaliyogawiwa kinyume cha sheria pamoja na kusitisha kwa muda shughuli za ugawaji wa viwanja katika eneo la Pangani hadi uhakiki utakapokamilika.






