Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Shinyanga
Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, Serikali inaandaa mradi maalumu wa kusambaza umeme katika maeneo ya uzalishaji, hususan maeneo yenye shughuli za uchimbaji wa madini, kwa lengo la kuwawezesha wazalishaji kutumia nishati ya uhakika na kupunguza utegemezi wa dizeli.
Mhe. Ndejembi ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mhe. Mabula Magangila, aliyeomba Serikali kupeleka umeme katika maeneo ya uzalishaji, akieleza kuwa baadhi ya wachimbaji madini katika jimbo hilo bado wanatumia dizeli kuendesha shughuli zao za uzalishaji.
Mbunge huyo pia ameieleza Serikali kuwa vitongoji 98 katika Jimbo la Msalala bado havijaunganishwa na huduma ya umeme.
Akijibu hoja hiyo, Mhe. Ndejembi amesema Serikali tayari imeanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo maalumu kwa kushirikiana na Wizara ya Madini, ambao utalenga kusogeza huduma ya umeme moja kwa moja kwenye maeneo yenye shughuli za uzalishaji, hususan maeneo ya migodi.
Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza tija katika uzalishaji, kupunguza gharama zinazotokana na matumizi ya dizeli pamoja na kuwawezesha wachimbaji na wazalishaji kutumia nishati ya umeme iliyo nafuu, ya uhakika na endelevu.
Kuhusu upatikanaji wa umeme vijijini katika Jimbo la Msalala, Mhe. Ndejembi amesema vijiji vyote tayari vimefikiwa na huduma ya umeme, huku Serikali ikiendelea na jitihada za kuwafikishia huduma hiyo wananchi waliopo katika vitongoji ambavyo bado havijaunganishwa, ikiwemo vitongoji 98 vilivyotajwa.
Aidha, akizungumzia upatikanaji wa umeme katika Jimbo la Kahama Mjini, Mhe. Ndejembi amesema tayari amefanya mazungumzo na Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Benjamini Ngaiwa, kwa lengo la kubainisha maeneo yaliyopo ndani ya Manispaa ya Kahama ambayo, licha ya kuwa ndani ya eneo la mjini, yana sifa na taswira za maeneo ya vijijini.
Amesema maeneo hayo yataangaliwa ili yaweze kunufaika na utaratibu wa Serikali wa kuunganishiwa umeme kwa gharama ya Shilingi 27,000 kwa mteja, kama ilivyoelekezwa.
Mhe. Ndejembi amesema Serikali itaendelea kuweka kipaumbele katika upanuzi wa miundombinu ya umeme na kuhakikisha nishati inafika katika maeneo yenye shughuli za kiuchumi na uzalishaji, ili kuongeza tija, kuchochea uwekezaji na kuboresha maisha ya wananchi.








