Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, ameongoza Mbio za Hisani za CRDB Bank International Marathon zilizofanyika katika Viwanja vya Posta Kijitonyama, Dar es Salaam, kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi wenye uhitaji.
Amesema kupitia mbio hizo, zaidi ya watoto 1,000 wamepatiwa matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), huku zaidi ya wanawake 450 wenye ujauzito hatarishi wakipatiwa huduma katika Hospitali ya CCBRT.
Amesema hatua hiyo imechangia kuokoa maisha ya wananchi ambao wangekabiliwa na madhara makubwa kutokana na changamoto za kiafya, akisisitiza kuwa Tanzania inahitaji rasilimali watu wenye afya njema, vijana wenye fursa pamoja na sekta binafsi zinazowajibika ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2050.
Mhe. Hemed amesema CRDB International Marathon inaendelea kuongeza nguvu katika vipaumbele vya Serikali kwenye sekta ya afya kwa mwaka 2025/2026, hususan katika kuimarisha huduma za kinga, afya ya uzazi pamoja na huduma kwa mama na mtoto, kwa lengo la kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
“Wadau mbalimbali na wananchi endeleeni kuunga mkono CRDB Marathon kwani fedha mnazochangia zinalenga kugusa maisha ya watu wenye uhitaji na kuboresha ustawi wa jamii kiafya,” amesema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Sambamba na hilo, ameupongeza CRDB Bank Foundation kwa kuwekeza katika maeneo yanayoendana na vipaumbele vya Serikali, akisema hatua hiyo ni mfano wa ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Naye Mkurugenzi wa CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema lengo la CRDB Bank International Marathon ni kubadili maisha ya Watanzania wanaokabiliwa na magonjwa mbalimbali, yakiwemo magonjwa ya moyo, saratani pamoja na changamoto za kiafya kwa wanawake wajawazito na watoto walio katika hali hatarishi.
Dkt. Nsekela amesema CRDB imejipanga kuendelea kutoa huduma kubwa zaidi kwa jamii, hususan vijana, wanawake na watoto, kwa kutambua kuwa uchumi imara hujengwa na watu wenye afya bora.
Amesema kupitia CRDB Bank International Marathon, watoto zaidi ya 400 tayari wamesaidiwa kupata huduma za upasuaji wa moyo, huku wanawake wenye ujauzito hatarishi wakisaidiwa kupata huduma na kujifungua salama.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank Foundation, CPA Oswald Urassa, amesema Benki ya CRDB imejikita katika kutoa miongozo ya kisera kwa Menejimenti ili kuhakikisha taasisi hiyo inawafikia walengwa kupitia programu mbalimbali ambazo tayari zimenufaisha maelfu ya Watanzania.
CPA Urassa amesema CRDB ina mkakati wa kuwa kinara katika utoaji wa huduma za kifedha katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku ikiendelea kuimarisha mahusiano na nchi jirani kwa lengo la kupanua huduma, kukuza uchumi na kuimarisha huduma za kihatarish.





