Na Mwamvua Mwinyi, Rufiji

Watanzania wametakiwa kuenzi juhudi za muasisi wa Taifa letu Bibi Titi Mohammed ambae alishiriki kumkomboa Mwanamke na kumng’oa mkoloni kwa maslahi ya Taifa na vizazi vijavyo.

Akimuelezea hayati Bibi Titi wakati wa Kongamano la kumuenzi muasisi huyo lililoandaliwa na Halmashauri ya wilaya ya Rufiji kwa kushirikiana na ofisi ya Mbunge Mohammed Mchengerwa, Mwenyekiti wa UWT Taifa Mary Chatanda alieleza , Mwanamke huyo alikuwa jasiri mwenye misimamo mikali kulipigania Taifa na kumkomboa mwanamke.

“Muasisi huyo atakumbukwa pamoja  na baba wa Taifa Mwl.Julius Nyerere kwa harakati zao za kulikomboa Taifa”amesema Chatanda .

Aidha alieleza Bibi Titi aliwahi kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania na amezidi kukumbukwa na Jumuiya ya wanawake kwa kuenzi yale aliyokuwa akiyafanya kwa vitendo.

“Leo hii tunamshuhudia Rais Samia Suluhu Hassan akifuata nyayo za Bibi Titi kwa kupigania usawa wa Maamuzi na uongozi kwa wanawake pamoja na kupambana na vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake”ameeleza Chatanda.

Awali mwanae Bibi Titi ,aliyejitambulisha kwa jina la Halima alisema , Bibi Titi ni mwanamke aliyejitoa mhanga kwa Ukombozi wa Watanzania.

Alisema ,pia alipenda haki kwa mwanamke ,na alipenda kuona mwanamke anashika nafasi mbalimbali za Uongozi hadi Urais .

“Cha ziada alikuwa nyakanga na mwana sanaa ,alikuwa na sauti nzuri, alikuwa na kipaji kutoka kwa kizazi chake ambapo aliimba wimbo wa Hongera Mwanangu na baadae wimbo huu kuwa maarufu baada ya Issa Matona kuuenzi na wimbo huo kuendelea kutamba hadi leo”ameelezea Halima.

Mwanasiasa mkongwe nchini Kate Kamba alieleza anavyomfahamu Bibi Titi Mohammed katika siasa, mwanaharakati kuwang’oa wakoloni pamoja na kumkomboa mtoto wa kike kupata elimu sawa .

Ameeleza Bibi Titi alikuwa mwanamke mwenye misimamo mikali ,na kutoa wanawake ndani kwenda kushiriki katika mikutano na siasa .

Kate amemuelezea ,muasisi huyo kuwa alikuwa shujaa ,mwenye maono makubwa kumkomboa mwanamke , mwanamke mwenye mipango na kupigania elimu kwa watoto wa kike na ndio maana alihakikisha wajukuu zake wanasoma.

“Tulimhangaikia mjukuu wake wa mwisho Dola kumpambania mjukuu wake huyo anasoma  Canada ,na wajukuu zake wote walisoma ,aliwalea kwa kuhakikisha wanasoma”amesema Kate.

Alifafanua,Jumuiya na Chama Cha Mapinduzi wafuate nyayo zake katika ujasiri wa kupita kuwavuta wanachama wapya, yeye aliweza kuwavuta wanachama zaidi ya 5,000 kujiunga na TANU na alifanikiwa.

Mjumbe wa mkutano Mkuu wa Jumuiya hiyo na ambaye pia ni mbaraza Mariam Ulega alisema ni jambo la faraja , Wanawake Mkoa wa Pwani kwa kufanya maadhimisho ya kumbukumbu hayo katika Mkoa huo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanawake ,Mkoa wa Pwani Zainabu Vulu amewapongeza Wanawake kwa jinsi ambavyo wamejitokeza katika maadhimisho hayo.

 Bibi Titi alizaliwa Mwaka 1926 na kufariki Nobemba 5, 2000  katika hospital ya Net Care iliyoko Johannesburg Afrika Kusini ambako alikuwa akitibiwa.

Moja kati ya barabara kubwa ya Jijini Dar es Salaam limepewa jina la Bibi Titi Mohammed kwa heshima ya kuenzi mafaniko makubwa na mchango wake wakati wa mbio za kutafuta uhuru wa Mtanzania.

By Jamhuri