IGP apangua makamanda, amuhamisha Mutafungwa

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Camillus Wambura, amewahamisha baadhi ya Makamanda wa Polisi kutoka katika nafasi zao na kuwapangia sehemu zingine.

kupitia taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Oktoba 20, 2022 na Msemaji wa Jeshi la Polisi SACP David Misime imeeleza kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ulrich Matei amepangiwa kuwa Mkuu wa Kitengo cha Polisi Wasaidizi na Kampuni Binafsi za Ulinzi nchini ambapo anachukuwa nafasi ya Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Issack Katamiti.

Pia, amewahamisha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Ng’anzi, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ambaye amehamishwa kwenda kuwa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania huku aliyekuwa Mkuu wa Kikosi hicho Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Wilbroad Mtafungwa, anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza.

Aidha, taarifa imeeleza kuwa aliyekuwa Afisa Mnadhimu Mkoa wa Kipolisi Rufiji Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Protus Mutayoba, amekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rufiji baada ya Kamanda wa Mkoa huo kuhamishiwa Mkoa wa Kipolisi Temeke hivi karibuni