Malkia Maxima wa Uholanzi ameipongeza Tanzania kwa ukuaji wa huduma jumuishi za fedha nchini ambapo idadi ya Watanzania wanaopata huduma za kifedha imepanda kutoka asilimia 17 kwa mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 58 kwa mwaka 2022.

Akizungumza alipokutana na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Florens Luoga leo jijini Dar es Salaam, Malkia Maxima ambaye pia ni Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Huduma Jumuishi za Fedha, alisema kuwa pamoja na kuongezeka kwa watumiaji wa huduma za kifedha nchini, idadi kubwa ya watanzania bado wanafanya malipo kwa kutumia pesa taslimu hivyo kupunguza ukuaji wa malipo ya kidijitali.

Malkia Maxima wa Uholanzi (kushoto) akizungumza katika wa kikao na Gavana, Prof. Florens Luoga kilichofanyika Benki Kuu Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Naibu Gavana Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Kassim Msemo na Naibu Gavana, Utawala na Udhibiti wa Ndani Bw. Julian Banzi Raphael. 

“Malipo ya kidijitali yatachochea ukuaji wa biashara, kuongeza uwazi na hata kuwezesha watumiaji wa huduma za kifedha kupata mikopo kwa urahisi” amesema.

Malkia Maxima ameongeza kuwa ili kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma za kifedha hadi asilimia 100 ni muhimu kuangalia kama wateja wanamudu gharama ya huduma za kifedha, namna ya kuhusisha sekta za kiuchumi kama kilimo pamoja jinsi gani mabenki na kampuni za mawasiliano zinatumia teknolojia kuleta mabadiliko.

Awali, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Florens Luoga ameeleza kuwa BoT inatayarisha mpango wa kuendeleza utekelezaji wa huduma jumuishi za fedha unaolenga kuongeza idadi ya wananchi wanaofikiwa na huduma za fedha nchini na kwa bei rahisi.

Malkia Maxima wa Uholanzi akifafanua jambo kuhusu Huduma Jumuishi za Fedha wakati wa wa kikao na Gavana, Prof. Florens Luoga kilichofanyika Benki Kuu Dar es Salaam

“Benki Kuu ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo utakaohakikisha kuwa huduma jumuishi za kifedha zinapatikana kwa urahisi au bila malipo” amesema.

Gavana Luoga aliongeza kuwa “kwa kushirikiana na timu maalum iliyoambatana na Malkia Maxima, kutakua na mpango wa tatu wa kuratibu jinsi gani ya kupanua wigo wakupeleka huduma jumuishi za kifedha kwa wananchi.

Malkia Maxima alikuja Tanzania mara ya kwanza mwaka 2010 wakati ambapo BoT inaanza mchakato wa kutekeleza huduma jumuishi za fedha. Pia alikuja 2013 na kuzindua mpango maalum wa kwanza utekelezaji wa huduma jumuishi za fedha.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Florens Luoga akielezea jambo katika kikao na Malkia Maxima wa Uholanzi kilichofanyika Benki Kuu Dar es Salaam
Malkia Maxima wa Uholanzi (katikati) akiteta jambo na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania , Prof. Florens Luoga. Kulia ni WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),Mhe. Angellah Kairuki. 

By Jamhuri