Na Mwandishi wetu Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi Nchini kupitia Kamisheni ya Polisi Jamii limekuja na mbinu ya kuzuia matukio ya uhalifu hususani ya mauaji pamoja na ya ukatili.

Kamishna wa Polisi Jamii Nchini CP.Faustine Shilogile wakati akizungumza na Maafisa, Wakaguzi na Askari wa Vyeo mbalimbali mkoani Arusha mapema leo amesema jeshi hilo kwa sasa limejipanga kuhakikisha linazuia matukio ya uhalifu kabla hayajatokea kwa kuwatumia wakaguzi wa Polisi ambao wamepangwa katika kata zote Nchini.

CP Shilogile amebainisha kuwa hivi karibuni kumeibuka matukio ya mauaji na ya ukatili wa kijinsia ambapo amesema sababu zikiwa ni pamoja na imani za kishirikina, migogoro ya ardhi pamoja na wivu wa mapenzi.

Kamishna Shilogile ameendelea kufafanua kuwa wakaguzi hao kupitia mafunzo mbalimbali waliyopewa wataenda kubaini viashiria vya uhalifu, kushauri na wakati mwingine kutoa taarifa mapema ili hatua za haraka zichukuliwe kabla ya uhalifu kutokea.

Aidha amewataka askari wote nchini kwenda kushirikiana na viongozi wa Serikali,wazee wa mila pamoja na viongozi wa dini ili wote kwa pamoja wakemee vitendo hivyo pamoja na kutoa elimu kwa wananchi ili kukomesha matukio hayo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo pamoja na kushukuru maelekezo na elimu waliyoipata kupitia kikao hicho amesema jeshi hilo mkoani humo litakwenda kuboresha utendaji wake wa kazi hali ambayo itapelekea kuwa na matokeo mazuri ndani ya taasisi na jamii yote kwa ujumla.

Naye Kadele Mabumba Meneja wa mradi Taasisi ya Hann’s Seidel ambao ni wadau wakubwa wa Jeshi la Polisi katika masuala ya amani na usalama amebainisha kuwa taasisi hiyo imewapa mafunzo askari mbalimbali wa Jeshi hilo na kuwataka kwenda kufuata maadili ya kazi ambayo yatapelekea kuwa na mafanikio katika kuzuia uhalifu.

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wahadhiri wa vyuo vikuu wapo katika ziara ya kutembelea mikoa yote nchini kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja baina ya jeshi hilo, Serikali na wananchi kuhusu umuhimu wa kushirikiana katika kufichua matukio ya uhalifu.

By Jamhuri