Wakala wa Vipimo Mkoa wa Dar es Salaam imeendeshaukaguzi wa kushtukiza kwenye maduka ya kuuzia nyama kwa lengo la kujiridhisha kama vipimo vinatumika kwa usahihi.

Takribani maduka 21 yamekaguliwa na mabucha manne yamebaini kufanya udanganyifu kwa kutokutumia vipimo kwa usahihi ili kuwapunja wanunuzi wa bidhaa hizo.

Akizungumza mara baada ya zoezi la ukaguzi wa kushtukiza Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA), Ilala Alban Kihullam amesema, kuwa zoezi hilo ni la kisheria na hufanyika muda wowote, siku yoyote na saa yoyote lengo likiwa ni kuangalia matumizi ya vipimo kama yanatumika kwa usahihi kwa mujibuwa Sheria.

Meneja Kihulla amesema,kwa ukaguzi uliofanyika watuhumiwa wamebainika kuwaibia wateja wao kiasi cha nusu kilo katika kila kilo mbili zinazonunuliwa na mabucha mengine yamekuwa yakiibia wateja kiasi cha gramu 250 kwenye kila kilo moja ya nyama.

Kihulla ameeleza kuwa, watuhumiwa wote waliokamatwa wamechukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura ya 340 Mapitio ya 2002 na marekebisho yake ili iwe funzo kwa wafanyabiashara wengine wenye tabia za kuchezea vipimo.

WMA imetoa wito kwa wananchi kuwa makini wanapokwenda kununua nyama kwenye maduka mbalimbali na kuwataka washiriki kwenye tukio la upimaji kuliko kuwaamini wauzaji na endapo watabaini changamoto yoyote wawasiliane nao kwa namba ya simu ya bila malipo ya 0800 110097 kwa msaada.

Kadharika, wito umetolewa kwa wauzaji wote wa nyama kuachana na tabia za kuvunja sheria kwa kuwaibia wateja wahakikishe wanatenda haki kwa kupima nyama kwa usahih ina kwenye mizani sahihi iliyohakikiwa kwani kinyume na kufamya hivyo wataondoa uaminifu kwa wateja wao na watachukuliwa hatua kali za Kisheria.

Vilevile,wamiliki wa bucha za nyama wametakiwa kufuatilia mwenendo wa biashara zinavyofanyika kwenye maeneo yao ya biashara kwa kuwa linapotokea tatizo lolote la wizi kwa kutotumia mizani kwa usahihi hawatakuwa salama na watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo.

By Jamhuri