*Ni tani 70,000 zilizokamatwa na kuthibitishwa ni feki

*Bodi ya Korosho yazirejesha kwa mzabuni zipelekwe kwa wakulima

*Mkurugenzi Mkuu CBT azungumza, asema zimejadiliwa Dodoma

Dar es Salaam

Na Alex Kazenga

Takriban tani 70,000 za viuatilifu aina ya ‘sulfur’ zilizokamatwa mkoani Lindi mwaka jana na kuthibitishwa kuwa ni feki, huenda zikarejeshwa sokoni; JAMHURI limedokezwa.

Uamuzi wa kurejeshwa sokoni kwa viuatilifu hivyo hatari unadaiwa kufanyika kutokana na udhaifu wa uongozi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT).

JAMHURI limeelezwa kuwa baada ya kukamatwa, sampuli zilichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi na Taasisi ya Viuatilifu (TPRI) ikathibitisha kuwa mzigo huo ulikuwa feki.

“Kwa maana hiyo, hii ‘sulfur’ (ya unga) ilipaswa kuharibiwa kwa kuwa TPRI imethibitisha kuwa ni feki, lakini kwa msaada wa Francis Alfred (Kaimu Mkurugenzi wa CBT) na vigogo wengine wa Wizara ya Kilimo, imerejeshwa kwa mzabuni.

“Barua rasmi na uamuzi wa kurejeshwa iliandikwa na Kaimu Mkurugenzi peke yake. Kwa sasa hiyo ‘sulfur’ inawekwa upya kwenye mifuko (repackaging) huko Masasi tayari kwa kusambazwa tena,” anasema mtoa habari wetu.

Barua ya kukabidhiwa mzigo huo kwa mzabuni (nakala tunayo) iliandikwa na CBT Septemba 27, 2021 ikiwa na kumbukumbu namba CBT/E/37/Vol.X1/5 na kusainiwa na Alfred.

Hali hii inatajwa kuwa ni kuhatarisha usalama wa wananchi na sekta ya kilimo cha korosho katika mikoa ya kusini, inayotajwa kugeuzwa dampo la viuatilifu visivyofaa.

Mbali na viuatilifu vya aina hiyo, uzembe wa CBT unadaiwa kusababisha wafanyabiashara kupeleka huko pembejeo zinazotumika kukuzia mboga badala ya zile za korosho.

CBT ipo taabani, yatuhumiwa kwa ubadhirifu

Bodi ya Korosho (CBT) inayosimamia zao namba moja katika kuchangia pato la taifa nchini, ipo mahututi kutokana na waliopewa dhamana ya kuisimamia kuendekeza migogoro na ubadhirifu wa fedha.

Uwepo wa pembejeo bandia na viuatilifu visivyokidhi viwango, hasa mkoani Mtwara, navyo vinatajwa kama vitu vingine vinavyokoleza moto kuiangamiza CBT na zao lake.

Wadau wa korosho na wafanyakazi kadhaa wa CBT wamelieleza JAMHURI kuwa iwapo mamlaka za juu hazitaingilia kati kunusuru hali hiyo, kuna kila dalili za kudorora kwa uzalishaji wa korosho.

Mmoja wa watoa taarifa amesema: “CBT kwa sasa ina hali mbaya. Inakabiliwa na migogoro inayochochewa na vigogo ndani ya bodi na wengine wapo Wizara ya Kilimo.

“Kinachosababisha yote haya ni masilahi binafsi na asilimia 10 wanazopata kutoka kwa wazabuni.”

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa ndani ya miaka sita kuanzia mwaka 2016, serikali imekuwa katika jitihada za kuikwamua CBT bila mafanikio.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2020/21, imebaini udhaifu mkubwa katika Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB), ikiuweka mwenendo wa korosho kama mfano.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa katika miaka minne iliyopita, uzalishaji wa korosho umeshuka kwa wastani wa asilimia 33.

Mwaka 2017/18 uzalishaji ulishuka kutoka tani 313,826.39 hadi tani 201,785.84 mwaka 2020/21. 

“Ni kama mkosi vile! Yaani kila mkurugenzi wa CBT anayeletwa, badala ya kuisaidia bodi kwa kusimamia kazi za kila siku za menejimenti, anaishia kuanzisha migogoro na kuingia kwenye ubadhirifu wa fedha tu,” anasema mtoa taarifa wetu (jina tunalihifadhi).

Ikumbukwe kuwa kuna kipindi Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, aliivunja Bodi ya Wakurugenzi ya CBT na kuiacha muda mrefu bila kuwa na uongozi.

Uamuzi huo ulitokana na kuthibitika kwa taarifa za uongozi uliokuwapo kukithiri kwa rushwa, ubadhirifu na migogoro.

Inadaiwa kuwa wajumbe wa bodi ya wakati huo walikuwa wakilipana mabilioni ya fedha kwa ajili ya vikao, huku bodi ikiwa kwenye mdororo.

Mkurugenzi wa bodi aliyekuwapo kabla ya bodi kufumuliwa, Profesa Wakuru Magigi, anadaiwa kufanya kazi bila kuelewana na wafanyakazi na maofisa wa serikali wa mikoa inayolima korosho.

Tabia zake zilisababisha kuibuka migogoro ndani ya bodi ambayo imerejea tena, sasa ikimhusisha Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Francis Alfred.

Kaimu Mkurugenzi ametoka wapi?

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Alfred, aliyekaimishwa ukurugenzi wa CBT, alipewa nafasi hiyo kimyakimya na Waziri wa Kilimo wa zamani, Japhet Hasunga, kuchukua nafasi ya Profesa Magigi aliyeondolewa na serikali, akitokea Songwe, mkoa anakotoka Hasunga.

Na sasa Alfred anadaiwa kuingia katika mkumbo ule ule wa Profesa Magigi, akihusishwa kwenye migogoro na ubadhirifu wa fedha unaotishia uhai wa CBT huku ikidaiwa kuwa kwa sasa hali ni mbaya kuliko wakati wa bodi ya awali.

Mgogoro mkubwa unaohusishwa na Alfred ni kuruhusu usambazaji wa viuatilifu visivyokidhi viwango na mbolea feki.

Mtoa taarifa wetu kutoka ndani ya CBT anasema: “Mwanzoni alianza vizuri, lakini baada ya kupata uzoefu akaanza mambo yale yale, na sasa ameigawa CBT vipande viwili; timu yake ndiyo huamua kila kitu bila kushirikisha vikao huku ikiwa na watu wasio na uelewa wa korosho, akiwaweka pembeni wataalamu.”

Kutokana na kutoelewana, inadaiwa kuwa watumishi wa vyeo vya juu wameikimbia CBT wakihofia kudhalilishwa na wenzao walio upande wa kaimu mkurugenzi mkuu.

Aliyetimuliwa na PM arejeshwa

JAMHURI linafahamu kwamba mwaka 2016, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alimwelekeza aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba, kumfukuza kazi mmoja wa watumishi wa CBT kwa tuhuma za ubadhirifu.

Lakini Alfred amemrejesha kazini, ikidaiwa kuwapo kwa vigogo ndani ya bodi na wizarani wamemtaka kufanya hivyo.

Mtumishi huyo (jina tunalihifadhi kwa kuwa hatujazungumza naye) anatajwa kama mtu anayeshirikiana na kaimu mkurugenzi mkuu kusababisha mivurugano.

Awali, ofisa huyo aliingia CBT Juni 2010 kwa ajira ya mkataba na ndani ya kipindi kifupi akapanda vyeo bila kufuata utaratibu.

Ofisa huyo alipanda vyeo mfululizo akiwa katika vituo vya Tunduru, mkoani Ruvuma na baadaye Tanga kabla ya kuondolewa kazini mwaka 2016.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa aliendelea kufanya kazi kwa mikataba ndani ya Wizara ya Kilimo kabla Alfred hajamrejesha CBT na kumpa mamlaka makubwa.

“Kwa sasa bila yeye kaimu mkurugenzi mkuu hafanyi uamuzi wowote. Kila kitu wanapanga wao. Tena nje ya vikao,” anasema ofisa mwingine wa CBT.

Mwongozo wa uchangiaji pembejeo kwa wakulima wa mwaka 2021 (110 mkulima, 110 mnunuzi) ni miongoni mwa mambo yaliyofanywa na wawili hao bila kushirikisha vikao kabla serikali haijaingilia kati.

“Hata mwaka huu pia, waliandaa mwongozo wa uchangiaji pembejeo kwa wakulima kupitia AMCOS na juzi juzi serikali imeagiza wakulima warejeshewe fedha zao,” amesema.

Na sasa yeye ni mmoja wa watia saini wa akaunti zote za CBT na taarifa zinasema mara kadhaa amekuwa akikaimu nafasi ya Alfred anapokuwa nje ya ofisi, huku wenye vyeo vya juu wakiwekwa pembeni.

Taarifa na malalamiko ya watumishi wa CBT yapo mezani kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho lakini hakuna hatua zilizochukuliwa.

Alfred azungumza

Akizungumza na JAMHURI, Kaimu Mkurugenzi wa CBT, Francis Alfred, amesema tuhuma zinazoelekezwa kwake hazina ukweli wowote huku akiweka sharti la kuzitolea ufafanuzi kwa kina endapo atatajiwa majina ya vyanzo vyetu vya habari.

“Hayo ni majungu ambayo hayana mbele wala nyuma, ni watu wanaozunguka na kunifitini mimi, kama wanazo taarifa za kweli wajitokeze hadharani waseme wazi, kwa nini wajifiche?” amehoji Alfred.

Hata hivyo, amegoma kuzungumzia masuala ya migogoro ndani ya bodi kwa njia ya simu, akidai kuwa mtu anayehitaji taarifa hizo anatakiwa kufika Mtwara na kufanya uchunguzi wa kina.

“Kama wanadai kuna ubadhirifu wa fedha za korosho, ofisi ziko wazi watu waje wachunguze, hakuna kitu cha siri, kila kitu kitawekwa wazi ikibainika ninaihujumu bodi nitaondolewa tu,” amesema.

Hata suala la ‘sulfur’ isiyofaa kuanza kusambazwa tena kwa wakulima, Alfred amesema hawezi kulizungumzia hilo na kudokeza kuwa kuna vikao vya tathmini vimefanyika Dodoma na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 300 kujadili pembejeo hizo.

“Kila kitu kimejadiliwa na najua ni kiasi gani kinapelekwa Mtwara na ni kwa nini, na kwenye hili kama kuna mtu anataka kufanya uchunguzi aje mwenyewe huku ataona kila kitu, si vimaneno vya kusikia sikia tu,” amesema Alfred.

Kwa upande mwingine Gazeti la JAMHURI limewatafuta TPRI kwa njia ya simu ya mkononi ili kufahamu kwa kina pembejeo aina ya ‘sulfur’ kiasi cha tani 70,000 inayodaiwa kuwa haifai, lakini mtumishi mmoja wa taasisi hiyo (jina tunalo) akadai kuwa hana taarifa.

“Sijui unamaanisha nini unaponiambia mambo ya ‘sulfur’ feki, kwanza, sijui ni kitu gani. Hata hivyo, mimi si mtu sahihi wa kuzungumzia suala hilo,” amesema mtumishi huyo huku akikata simu na kutoweka hewani.

By Jamhuri