Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema kuwa duniani kuna mifumo mitatu ya usimamizi wa vyombo vya habari ambapo kila Serikali huamua kuchagua mfumo mmoja ambao utawaunganisha na wana habari.

Hayo ameyabainisha leo katika Kipindi cha Mezani kinachorushwa na Kituo cha Redio cha EFM, jijini Dar es Salaam.

“Mfumo wa kwanza ni self regulation, mfumo wa pili ni serikali ‘kushika’ vyombo vya habari kama ilivyo sasa na mfumo wa tatu ni co-regulation ambapo serikali na wadau wa habari wanakuwa na chombo ambacho kinawaunganisha.

“Sisi sekta ya habari tunataka huu mfumo wa tatu ambao ndio tunaupigania, sio ule wa Serikali kuwa mlalamikaji, msuluhishi na hakimu. Huu mfumo utazikwa kwa kuunda Baraza la Huru la Vyombo vya Habari,” amesema Balile.

Balile amesema,haki ya uhai haipo kwenye mikono ya mwanadamu yeyote lakini haki ya habari inapangwa na wanadamu namna ya kuitumia

“Tunataka sheria hizi za habari zitupe mwongozo wa msingi.Baada ya haki ya uhahi, kinachofuata ni haki ya kupata habari,” ameongeza.

Amesema, TEF kwa kushirikiana na wadau wa habari nchini, wanapendelea mfumo wa tatu ambao unatoa fursa kwa pande zote mbili (wadau na serikali) kuwa na sehemu ya kukutana pale kunapokuwa na malalamiko.

Akizungumzia ushirikishwaji wa wanahabari wenyewe kwenye mabadiliko hayo, Balile amesema wamekuwa na mikutano ya mara kwa mara na wanahabari katika kuwafafanulia vifungu hivyo.

Na kwamba, TEF imekuwa ikifanya mikutano na wahariri, waandishi pamoja na waandishi wa habari za mtandaoni (online contents).

“Vikao hivi tumevifanya mara kwa mara na waandishi wanaelewa, na hatua iliyopo sasa ni kwenda kwenye mjadala ulioitishwa na Wizara ya Habari, Mawasilia na Teknolojia ya Habari tarehe 11 hadi 12 Agosti mwaka huu kwa ajili ya kupitia vifungu vinavyolalamiukiwa,” amesema.

By Jamhuri