Na Mwandishi Maalum,JamhuriMedia

Wapiga Kura 74,642 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 13 za Tanzania Bara kesho Julai 13,2023.

Jumla ya wapiga kura 74,642 walioandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huu mdogo na jumla ya vituo 205 vya kupigia kura vitatumika.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegele katika Risala ya Uchaguzi huo mdogo unaofanyika kujaza nafasi wazi za udiwani.

Jaji wa Rufaa Mwambelegele amewataka wasimamizi wa uchaguzi, vyama vya siasa na wagombea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi wakati wa Uchaguzi Mdogo wa madiwani katika Kata 13 za Tanzania Bara.

Uchaguzi huo mdogo utashirikisha, Kata ya Ngoywa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Kata ya Kalola katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mkoani Tabora na za Sindeni katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Potwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Kwashemshi katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Bosha katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga zote za Mkoa wa Tanga.

Kata nyingine ni Mahege katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti mkoa wa Pwani, Kata ya Bunamhala katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi, mkoa wa Simiyu, Kata ya Njoro na Kalemawe zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kata ya Kinyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Makete mkoa wa Njombe , Kata ya Magubike katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro na Kata ya Mbede katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoa wa Katavi.

Aidha,amevitaka vyama vya siasa, wagombea na wadau wa uchaguzi kuepuka kujihusisha na matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani kwani jukumu la kulinda amani ni la kila mmoja, hivyo wahakikishe wanalinda amani iliyopo nchini.

“Jukumu la kulinda amani ya nchi yetu ni la kila mmoja wetu wakiwemo wananchi, vyama vya siasa, wagombea na wadau wengine wa uchaguzi,”alisema Jaji wa Rufaa Mwambegele.

Aliongeza kuwa Sheria na Kanuni za Uchaguzi zimeweka mamlaka na taratibu zinazotakiwa kufuatwa iwapo kutakuwepo na malalamiko yoyote wakati wa uchaguzi, hivyo amevitaka vyama vya siasa na wagombea kufuata taratibu hizo ili uchaguzi huo ufanyike kwa uhuru na haki.

Mweyekiti huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi amewataka wapiga kura wote waliojiandikisha katika Kata 13 za Tanzania Bara kujitokeza kupiga kura ili waweze kuwachagua madiwani wanaowataka.

Amevitaka vyama vya siasa wagombea na wafuasi wao kuzingatia kuwa kampeni za uchaguzi zinakamilika leo Julai 12,2023 saa 12:00 jioni hivyo hawaruhusiwi kufanya mikutano ya kampeni kuanzia muda huo na hawaruhusiwi kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni kama vile vipeperushi, bendera na mavazi.

Aidha Jaji Rufaa Mwambegele amevikumbusha vyama vya Siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo, kuzingatia wajibu wao wa kuweka mawakala katika vituo vyote vya kupigia, kuhesabu na kujumlishia kura.

“Upigaji kura utafanyika katika vituo vile vile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni. Iwapo watakuwepo wapiga kura katika mstari ambao walifikakabla ya saa 10:00 jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura, mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya saa 10:00 jioni”alisema Jaji Rufaa Mwambegele.

Aliongeza “Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 62(1) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura 292, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao au kadi kuharibika kutumia vitambulisho mbadala”.

Amevitaja vitambulisho mbadala kuwa ni Passi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).

Mpiga kura aliyepoteza kadi au kadi yake kuharibika ataruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala iwapo tu atakuwa ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na jina lake lipo kwenye orodha ya wapiga kura kwenye kituo anachopigia kura.

Mwambegele amekumbusha kuwa katika vituo vya kupigia kura kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha watakaokuwa na watoto vituoni na kutakuwa na majalada ya nukta nundu katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa kuona ili weweze kupiga kura wenyewe.

Alifafanua kuwa kwa wapiga kura wenye ulemavu wa kuona ambao hawawezi kutumia majalada hayo wanaruhusiwa kwenda vituoni na watu watakaowachagua wenyewe kwa ajili ya kuwasaidia kupiga kura.

Jumla ya vyama vya siasa 17 vimesimamisha wagombea katika uchaguzi huo mdogo ambapo Tume imevipongeza vyama hivyo na wagombea wao kwa kutumia haki yao ya msingi ya kikatiba kujitokeza kushiriki katika uchaguzi huo mdogo wa Udiwani.

By Jamhuri