Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
WIZARA ya Maliasili na Utalii itaendelea kutumia teknolojia katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kwa kununua ndege nyuki (drones) 12 na mikanda maalum ya mawasiliano 50 (GPS Satellite Collars) kwa ajili ya ufuatiliaji wa mienendo ya wanyamapori hao.
Hayo yameelezwa leo bungeni Mei 19,2025 na Waziri wa Wizara hiyo Dk Pindi Chana wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Waziri Chana amesema Mikanda hiyo itafungwa kwa tembo viongozi katika maeneo yenye changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Vilevile, Wizara itanunua na kusambaza mabomu baridi 40,000 katika maeneo yenye changamoto ya Tembo.
“Wizara itaendelea kufanya tafiti za kimkakati kwa ajili ya kugundua mbinu mpya za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.”amesema Dkt.Chana


Katika uwasilishwaji wa bajeti hiyo Kamishna Kuji ameongozana na Makamanda wa Kanda nne pamoja na Makamishna wengine Waandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).


