Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ameupongeza uongozi wa Shirikisho la Kimataifa la Watayarishaji wa Muziki Duniani (IFPI) kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano wao mkuu uliofanyika leo Jijini Dar es salaam.

Mwinjuma ametoa pongezi hizo leo Machi 26, 2024 alipokuwa akifungua mkutano huo ambapo amesema, uamuzi huo ni kutokana na kuimarika kwa usimamizi wa hakimiliki hapa nchini.

“Katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan yamefanyika mageuzi makubwa, ikiwemo mabadiliko ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki kwa lengo la kuhakikisha Wasanii wananufaika na kazi zao na Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) wamefanya jitihada mbalimbali za kuimarisha mahusiano ya Kimataifa katika usimamizi wa hakimiliki,” amesema Mwinjuma.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki, Doreen Anthony Sinare amesema mkutano huo, umelenga kuweka msisitizo wa viwango vya makusanyo ya mirabaha katika Redio na Televisheni kwa kuhakikisha wanalipia matumizi ya kazi za muziki na kuwa na makubaliano ya viwango vya makusanyo ambavyo havitofautiani sana.

“IFPI ni Shirikisho linalojihusisha na kusimamia haki za Watayarishaji wa Muziki na wamekuwa na utaratibu wa kuendesha mikutano yao katika nchi mbalimbali na hivi karibuni COSOTA tuliwaalika kufanya mkutano Mkuu wao Tanzania na waliridhia, kwa mkutano huu kufanyika nchini kutakuwepo na manufaa mengi kwa Watayarishaji wa muziki nchini pamoja na kubadilishana uzoefu wa usimamizi wa hakimiliki kutoka nchi mbalimbali,” amesema Doreen.

Aidha, Bi. Doreen amebainisha kuwa hivi sasa nchi nyingi za Bara la Afrika zimekuwa zinapewa ushirikiano na viongozi wa kisiasa katika kuimarisha usimamizi wa hakimiliki ikiwemo Tanzania hivyo wamesisitiza kutumia fursa hiyo.

Naye Mratibu wa Mkutano huo kutoka IFPI Bi. Angela Ndambuki ameipongeza Tanzania kwa kuandaa mkutano huo na kueleza kuwa, kufanyika kwa mkutano huo nchini kutasaidia kuendelea kutangaza Muziki wa Tanzania katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara na kufungua fursa mbalimbali kwa Watayarishaji wa Muziki wa Tanzania pamoja na Wasanii.

Share this Article

Facebook Twitter

Previous Article KAMATI YA LAAC IMEPONGEZA MRADI WA JENGO LA DHARULA HOSPITALI YA WILAYA YA SIMIYU NA UJENZI WA KIWANDA CHA KUTENGENEZA CHAKI

Next Article ZAIDI YA WANAKIJIJI 4000 WA KATA YA MAGILA GEREZA KUANZA KUPATA MAJI SAFI YA BOMBA

By Jamhuri