Serikali yathibitisha visa 64 vya UVIKO -19

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Serikali imesema katika kipindi cha kuanzia Aprili 22 hadi Mei 26,2023 jumla ya visa vipya 64 vilithibitika kuwa na maambukizi ya UVIKO -19 ikilinganishwa na visa vipya 45 vilivyothibitika wiki nne zilizopita,idadi hii ni sawa na ongezeko la visa vipya kwa asilimia 42.2.

Aidha katika kipindi hicho chote, Serikali imesema hakuna mgonjwa ambaye alilazwa au kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa UVIKO -19.

Kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Ahmad Makuwani amesema Serikali imeendelea kuimarisha udhibiti wa ugonjwa huo nchini huku ikiendelea kutoa taarifa juu ya mwenendo wa ugonjwa huo.

Amesema mbali na kutoa taarifa pia Serikali imeendelea kutoa huduma za chanjo ya UVIKO -19 nchini ili kuwawezesha wananchi kupata kinga kamili na hivyo kuzuia kupata ugonjwa mkali na hata kifo pale mtu anapopata maambukizi ya virusi vinavyosababisha UVIKO-19.

Amesema hadi kufikia Mei 26,2023 jumla ya watu 32.763.672 ambayo ni sawa na asilimia 106.6 ya walengwa ambapo watu wenye umri wa miaka 18 na zaidi walikuwa wamepata dozi kamili ya chanjo ya UVIKO-19 ambao ni sawa na asilimia 55 ya watanzania 59,851,347 waishio Tanzania bara.

‘’Wizara inaendelea kufuatilia kwa ukaribu hali ya UVIKO-19 nchini na duniani pamojana kutoa taarifa kwa umma na kuchukua hatua zaidi za udhibiti,pia wizara inahimiza watu wote wenye dalili za magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa kama vile homa,mafua,kikohozi,mwili kuchoka,maumivu ya viungo ,kuumwa kichwa ,vidonda vya koo,kupumua kwa shida kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mapema ili kuweza kupimwa na kupatiwa matibabu stahiki,’’alisema.

Dkt. Makuwani alisema wizara inaendelea kutoa tahadharoi kwa wananchi wote kuchukua hatua za kujikinga na UVIKO -19 na magonjwa mengine ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na kupata dozi kamili za chanjo ya UVIKO 19,Kuvaa barakoa pindi unapokuwa na dalili za mafua au kikohozi na uwapo kwenye mikusanyiko ,kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara kwa mara pamoja na kuendelea kuchukua hatua za kuimarisha mwili kwa kufanya mazoezi.