SERIKALI imesaini makubaliano na Benki ya Dunia ya Mkopo Nafuu wa sh. Trilioni 1.24 kwa ajili ya miradi ya umeme vijijini na ujenzi wa uendelezaji wa bonde la Mto Msimbazi utakaohusisha daraja la kisasa la Jangwani.

Ujenzi wa daraja la kisasa la Jangwani, unatajwa kuaandika historia nyingine ya daraja bora na la aina yake kama la Tanzanite lililopo baharini litakalojengwa Jangwani, hivyo wakazi wa Dar es Salaam kusahau adha ya mafuriko.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, mara baada ya makubalino hayo, Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba, amesema mikataba hiyo miwili yenye gharama ya dola milioni 535 sawa na sh trilioni 1.24 itaandika historia na kukuza uchumi wa nchi.

“ Huu ni mwanzo kati ya yale makubwa ambayo Rais Samia anatarajia kufanya katika mwaka huu wa fedha ikihusisha ujenzi wa miradi ya miundombinu jijini Dar es Salaam,”alisema.

Ameongeza kuwa, hatua hiyo ni mwendelezo wa kuaminika kwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kimataifa, ambapo kwa sasa nchi inaaminika zaidi hali inayosababisha majadiliano ya fedha na uendelezwaji wa miradi ya kiuchumi kukubalika kila sehemu.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila, alisema ujenzi wa daraja la juu la kisasa litakalofanana na la Tanzanite lililopo baharini au la Nyerere Kigamboni utaandika historia mpya ya kusahau adha ya mafuriko maeneo ya Jangwani.

Amesema ujenzi huo utakuwa wa daraja la mita 390 na litainuka kwa mita sita na kuhusisha upanuzi wa mto kwa kilomita 1.8 juu na kilomita 1.8 chini na kujengewa kingo za zege pembeni.

“ Ujenzi utagharimu zaidi ya dola milioni 63.3 na hivi karibuni tunatarajia kutangaza tenda ambapo baada ya miezi mitatu hatua za awali zitakuwa zimekamilika,”alisema.

Mativila ameeleza kuwa usanifu wa ujenzi umekamilika ambapo michoro inaonyesha kuwapo na daraja la kisasa utakaohusisha kuondolewa kituo cha mabasi ya mwendokasi Jangwani ambacho kitahamishiwa Ubungo Maziwa.

Hivyo, alisema matarajiao ni kuanza ujenzi huo Aprili mwakani na kukamilika baada ya miaka miwili hadi mitatu na kuondoa adha kubwa ya usafiri na usafirishaji kwa wananchi.
Mama msaada wako huko.

By Jamhuri