Wadau wa habari wana shauku kubwa ya kusikiliza muswada wa sheria ya habari ukisomwa kwa mara ya kwanza katika Bunge la Januari hii.

Akizungumza leo Januari 19,2023 jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deodatus Balile, amesema
mwelekeo ni mzuri na maelekezo ya Rais Samia yanatekelezwa na shauku wa wadau wa habari kuona mswada huo unaingia bungeni

Amesema kuwa mwezi huu wanatarajia kwamba Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itawasilisha muswada wa huduma za habari bungeni kama waziri alivyoahidi (Nape Nnauye) mara kadhaa kwamba utaingia bungeni na kujadiliwa.

“In sha Allah Mungu akipenda mwezi Februari itakuwa imepitishwa na kuwa sheria basi tutaanza utaratibu mwingine wa kuunda vyombo vinavyotakiwa ikiwemo Baraza Huru la Habari, na utunzi wa kanuni zitakazokuwa zimetokana na mabadiliko mbalimbali” amesema.

“Tunaona mwekelekeo ni mzuri na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanatekelezwa sasa na hamu yetu kubwa ni kuona muswada huo unaingia bungeni baada ya kushindikana katika Bunge la Februri mwaka jana,ukashindikana mwezi wa tisa,ukashindikana mwezi wa 11 .

“Lakini sasa tulishazungumza na Waziri,watendaji wa serikali ni matumaini yetu makubwa sana sana tunataraji kuona mswada huo ukiingia bungeni na mambo yote yaweze kwenda vyema,” amesema.

By Jamhuri